Revelation of John 7

Waisraeli 144,000 Watiwa Muhuri

1 aBaada ya hili nikaona malaika wanne wakiwa wamesimama katika pembe nne za dunia, wakizuia hizo pepo nne za dunia, ili kwamba pasiwe na upepo utakaovuma juu ya nchi au juu ya bahari au juu ya mti wowote. 2 bNikaona malaika mwingine akipanda kutoka mawio ya jua akiwa na muhuri wa Mungu aliye hai. Akawaita kwa sauti kubwa wale malaika wanne waliokuwa wamepewa mamlaka ya kuidhuru nchi na bahari, akisema, 3 c“Msiidhuru nchi wala bahari, wala miti, hadi tuwe tumetia muhuri kwenye vipaji vya nyuso za watumishi wa Mungu wetu.” 4 dNdipo nikasikia idadi ya wale waliotiwa muhuri: yaani 144,000 kutoka makabila yote ya Israeli.


5 Kutoka kabila la Yuda 12,000 walitiwa muhuri,
kutoka kabila la Reubeni 12,000,
kutoka kabila la Gadi 12,000,

6 kutoka kabila la Asheri 12,000,
kutoka kabila la Naftali 12,000,
kutoka kabila la Manase 12,000,

7 kutoka kabila la Simeoni 12,000,
kutoka kabila la Lawi 12,000,
kutoka kabila la Isakari 12,000,

8 kutoka kabila la Zabuloni 12,000,
kutoka kabila la Yusufu 12,000,
na kutoka kabila la Benyamini 12,000.

Umati Mkubwa Wa Watu Kutoka Mataifa Yote

9 eBaada ya hili nikatazama na hapo mbele yangu palikuwa na umati mkubwa wa watu ambao hakuna yeyote awezaye kuuhesabu, kutoka kila taifa, kila kabila, kila jamaa na kila lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi na mbele ya Mwana-Kondoo. Walikuwa wamevaa mavazi meupe na wakiwa wameshika matawi ya mitende mikononi mwao. 10 fNao walikuwa wakipiga kelele kwa sauti kubwa wakisema: “Wokovu una Mungu wetu,
yeye aketiye kwenye kiti cha enzi,
na Mwana-Kondoo!”

11 gMalaika wote walikuwa wamesimama kukizunguka kile kiti cha enzi na wale wazee ishirini na wanne na wale viumbe wanne wenye uhai. Wakaanguka kifudifudi mbele ya hicho kiti cha enzi na kumwabudu Mungu, 12 hwakisema: “Amen!
Sifa na utukufu
na hekima na shukrani na heshima
na uweza na nguvu
viwe kwa Mungu wetu milele na milele.
Amen!”

13 iKisha mmoja wa wale wazee ishirini na wanne akaniuliza, “Ni nani hawa waliovaa mavazi meupe, nao wametoka wapi?”

14 jNikamjibu, “Bwana, wewe wajua.”

Naye akasema, “Hawa ni wale waliotoka katika ile dhiki kuu, nao wamefua mavazi yao katika damu ya Mwana-Kondoo na kuyafanya meupe kabisa.
15 kKwa hiyo, “Wako mbele ya kiti cha enzi cha Mungu
na kumtumikia usiku na mchana
katika hekalu lake;
naye aketiye katika kile kiti cha enzi
atatanda hema yake juu yao.

16 lKamwe hawataona njaa
wala kiu tena.
Jua halitawapiga
wala joto lolote liunguzalo.

17 mKwa maana Mwana-Kondoo
aliyeko katikati ya kile kiti cha enzi
atakuwa Mchungaji wao;
naye atawaongoza kwenda
kwenye chemchemi za maji yaliyo hai.
Naye Mungu atafuta kila chozi
kutoka macho yao.”
Copyright information for SwhKC